Mbeya on Focus

Mbeya on Focus

Share

28/09/2024

POLISI WATEKA WAFANYABIASHARA NA KUPORA FEDHA

Jeshi la Polisi wilayani Mbarali mkoani Mbeya limewateka na kupora mamilioni ya fedha wakulima wawili ambao pia ni wafanyabiashara wa mpunga katika kijiji cha Ubaruku.

Tukio hilo limefanyika Julai mwaka 2023 na kundi la polisi wakiongozwa na Afisa Upelelezi wa Wilaya ya Mbarali OCCID Ndaki Abel ambaye alimteka mkulima na mfanyabiashara Magesa Charles Lugwisha akiwa kwenye shughuli zake za kununua mpunga maeneo ya Ifakara mjini na kusafirishwa hadi kituo cha polisi Rujewa.

Mfanyabiashara mwingine aitwaye Kumbusho Jonas Homange naye alitekwa akiwa kwenye shughuli zake Kijiji cha Ubaruku na kupelekwa eneo maalumu la mateso polisi na kushushiwa kipigo, wakamtishia kipigo zaidi k**a ambavyo mfanyabiashara mwenzie Magesa Charles Lugwisha amefanyiwa kwa lengo la kumshurutisha atoe fedha.

Baada ya wafanyabiashara hao kuona mateso yamezidi wakaamua kuchangishana fedha ili kuwapa askari kwa lengo la kuepukana na mateso makali waliokuwa wanayapata na waliambiwa kuwa wakitoa fedha hizo wataachiwa huru.

Awali askari walitaka wapewe milioni 60 lakini Magesa Charles Lugwisha akatoa kiasi cha shilingi Milioni 10 na Kumbusho Jonas Homange akatoa shilingi millioni 30 na wakapata jumla ya shilingi milioni 40 ambazo walimkabidhi Ndaki Abel ambaye alituma mtu wake wa karibu kuchukua fedha hizo kwa niaba yake.

Wafanyabiashara Kumbusho Jonas Homange na Magesa Charles Lugwisha wakati wote wakiwa mikononi mwa polisi hawajawahi kumwambiwa makosa yao zaidi ya kuwapigwa na kuwataka watoe fedha na kuwapa askari hao.

"Tulipigwa na polisi na wakatutishia ya kwamba tusitoe taarifa hizi mahali popote la sivyo tutafilisiwa mali zote na kuuwawa." alisema Kumbusho Homange

"Baada ya vipigo na kuumizwa niliendelea kutibiwa nyumbani kwa usimamizi wa Afisa Upelelezi wa Wilaya ya Mbarali OCCID aitwaye Ndaki Abel." alisema Magesa Lugwisha.

Gazeti la Mwanahalisi la tarehe 28 Machi 2024 liliripoti kwa kina juu ya sakata hili kwenye ukurasa wake wa 2 na 3 na kupelekea Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera kuunda Tume ya uchunguzi juu ya tukio hilo la uporaji wa fedha za wafanyabiashara.

Tume hiyo ilihusisha maafisa kutoka vyombo mbali mbali vya serikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kukupambana na Rushwa (TAKUKURU) Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Tume ilibaini ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, kuvunjwa kwa maadili ya utumishi kwa maafisa wa jeshi la polisi na makosa mengine ya jinai ikiwemo utekaji, uporaji na shambulio lenye nia ya kudhuru mwili kwa askari na maafisa wengine wa jeshi la polisi.

Aidha tume hiyo ilibaini uwepo wa ushirikiano kati ya mfanyabiashara aitwaye Milele Dembalemba Kaponda ambaye alishirikiana na afisa upelelezi wa wilaya ya Mbarali OCCID Ndaki Abel kupora fedha kwa wafanyabiashara hao.

Hivyo tume iliagiza kesi ya zilizofunguliwa na Ndaki Abel zifutwe na askari waliohusika kwa utekaji na unyanyanganyi kwa kutumia nguvu wahamishwe na washushwe vyeo na fedha zilizoporwa kiasi cha shilingi milioni 40 zirejeshwe kwa wafanyabiashara.

Ni miezi sita sasa tangu agizo hilo la tume dhidi ya idara ya polisi halijatekelezwa na wafanyabiashara hao wanapojaribu kufuatilia fedha hizo wanatishiwa maisha pamoja na biashara zao.

Kuna mkanganyiko wa taarifa kutoka kwa mamlaka zinazoshughulikia suala hilo kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Idara ya Usalama wa Taifa Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya na Wizara ya Mambo ya ndani ambapo ofisi zote hizi zinakwepa kushughulikia suala hili.

Hali hii imepelekea wahusika waliobainishwa na tume kuhusika na sakata hili kuendelea kutoa vitisho kwa wafanyabiashara walioumizwa na kuporwa fedha zao kuwa hakuna mamlaka inayoweza kuwasikiliza hivyo wanapoteza muda na fedha zaidi kuendelea kufuatilia fedha zao.

Bado kuna hofu imetanda kwa wakulima na wafanyabiashara wa mpunga wilayani Mbarali ambao wanafuatilia kwa karibu namna mamlaka za serikali zinavyoshughulikia sakata hili huku wakionyesha kutokuwa na imani namna mwenendo wa shauri hili unavyoendeshwa.

Hivi wizara imeshindwa kumaliza suala hili? Nini kinaendelea nyuma ya suala hili? Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pamoja na vyombo vya ulinzi na Usalama vimeshindwa kuwawajibisha wahusika wa unyama huu unaofanywa na jeshi la polisi?

Mamlaka zinazohusika wanasubiri Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati sakata hili ili haki itendeke? Hivi hawa wafanyabiashara wangebainika kuwa wanafanya biashara haramu, Je mamlaka zingeendelea kukaa kimya?

Ni nani aliwatuma hawa polisi kuteka na kupora fedha? Kwanini hawa askari wamehamishwa na wengine kushushwa vyeo badala ya kufukuzwa kazi? Kuna nini Mbarali Mbeya?

Kwenye sakata hili kila mtu anashangaa! Waziri wa mambo ya ndani anashangaa! Mkuu wa Mkoa anashangaa! Jeshi la polisi linashangaa! Mamlaka za usalama mkoa wa Mbeya zinashangaa! wakulima na wafanyabiashara wa mpunga waliotekwa na kuporwa fedha zao wanashangaa! wananchi wameduaa na kuchanganyikiwa!

Want your public figure to be the top-listed Public Figure in Mbeya?
Click here to claim your Sponsored Listing.

Category

Culinary Team

Attire

Website

Address


Mbeya