Mbeya Zonal Referral Hospital
03/06/2026
HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA YA MBEYA (MZRH) NA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA (TPA) ZAINGIA MAKUBALIANO YA KUWAPATIA WAFANYAKAZI TPA HUDUMA ZA MATIBABU YA DARAJA LA JUU
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zimesaini rasmi makubaliano ya kutoa huduma za matibabu ya kibobezi na daraja la juu (VIP) kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo, huku hospitali ikitangaza mapinduzi makubwa ya kimatibabu yaliyolenga kuifanya kuwa kituo kikuu cha tiba utalii kwa nchi za SADC.
Hatua hiyo imefikiwa leo, Juni 3, 2026, baada ya pande zote mbili kuridhia na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) pamoja na Mkataba wa Kiwango cha Huduma (SLA). Nyaraka hizo zimesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MZRH, Dkt. Godlove Mbwanji, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbosa mara baada ya kuwasilishwa na Mashaka Karume, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika mapema leo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji ameelezea kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya mikakati ya hospitali hiyo kusogeza huduma za afya maeneo ya kazi, sambamba na kuonyesha maboresho makubwa ya kibingwa yaliyofanyika katika kuanzishwa kwa upasuaji wa moyo na kukaribia kukamilika kwa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa mishipa ya damu (Cathlab), Kuimarika kwa huduma za upasuaji wa ubongo, moyo na mishipa ya fahamu pamoja huduma za kibingwa za kubadilisha na kupandikiza nyonga na magoti.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ndg. Mashaka Karume, amebainisha kuwa mkataba huo unaenda kuleta mageuzi makubwa kiutendaji kwa kuondoa vikwazo vya kiafya vinavyowakabili wafanyakazi wa mamlaka hiyo, hasa wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
03/06/2026
Menejimenti na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya tunakupongeza Bi. Ummy Mwalimu kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mshauri wa Rais katika Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto. Kila la heri katika majukumu yako mapya.
28/05/2026
MZRH KUSOGEZA HUDUMA ZA UPANDIKIZI WA MIMBA (IVF) MBEYA, KULENGA SOKO LA SADC
Mkuu wa Kitengo cha Wazazi na Watoto na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dkt. France Rwegoshora, amepongeza ubunifu na kiwango cha juu cha utoaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto zinazotolewa na wataalamu katika maonesho ya nne ya biashara na uwekezaji ya Mbeya City Expo 2026.
Dkt. France ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Mei 28, 2026, alipotembelea banda la maonesho la MZRH lililopo katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya na kupata fursa ya kuzungumza na watumishi waliopo mstari wa mbele kuwahudumia wananchi.
Dkt. France ameeleza kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya inakamilisha maandalizi makubwa na imejipanga kikamilifu kuanza kutoa huduma za kibingwa za upandikizi wa mimba (In Vitro Fertilization - IVF) baada ya maboresho makubwa ya miundombinu ya afya ya uzazi.
Amesema mkakati huu unalenga kutatua changamoto za uzazi na utasa kwa wanandoa na akina mama ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo jijini Dar es Salaam au nje ya nchi kwa gharama kubwa sana.
Dkt. Rwegoshora ameeleza kuwa maboresho hayo ya kihistoria hayatanufaisha tu wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Rukwa, na Katavi), bali yamepanuliwa kimkakati ili kuhudumia wananchi wa nchi zinazozunguka Tanzania katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC).
"Mbeya ni lango kuu la kijiografia. Hospitali yetu imejipanga kuwa kituo kikuu cha utalii wa kimatibabu (Medical Tourism) kwa majirani zetu wa nchi za SADC k**a vile Zambia, Malawi, DRC, na Msumbiji. Sasa raia wa nchi hizi hawatakuwa na sababu ya kwenda mbali; huduma zote za kibingwa za upandikizi wa mimba na matibabu ya kisasa ya uzazi yanapatikana hapa hapa Mbeya kwa viwango vya kimataifa," alisema Dkt. France.
Ameeleza kuwa mafanikio haya makubwa ni matokeo ya maono na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Serikali imeendelea kuwekeza mabilioni ya fedha katika ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya maabara za uzazi, mafunzo ya kibingwa kwa madaktari, na ujenzi wa majengo ya kisasa ya wazazi na watoto.
"Nimefarijika sana kuona jinsi watumishi wetu wanavyojitolea kwa weledi mkubwa kutoa elimu na ushauri kuhusu huduma hizi mpya hapa viwanjani. Haya ni mapinduzi makubwa yanayoakisi uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha ustawi na afya ya mama na mtoto nchini," aliongeza.
Katika hatua nyingine, Dkt. France ametoa wito thabiti kwa wananchi wote, mashirika, na wageni kutoka nchi jirani wanaotembelea maonesho hayo, kujitokeza kwa wingi kwenye banda la MZRH.
Alisisitiza kuwa uwepo wa madaktari bingwa na wataalamu wa mifumo ya uzazi kwenye banda hilo ni fursa ya kipekee ya kupata ushauri wa kibingwa bila malipo, kufanya uchunguzi wa awali, na kuelewa hatua za kufuata ili kunufaika na huduma hizi mpya na za kisasa za uzazi.
28/05/2026
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb), akipata maelezo baada ya kutembelea banda la Hospitali ya Rufaa ya Kanda katika maonesho ya Mbeya City Expo 2026.
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa jamii kwa kuhakikisha huduma bora na za kibingwa zinawafikia wananchi wote, hasa makundi maalum.
Click here to claim your Sponsored Listing.
Category
Contact the organization
Website
Address
Hospital Street
Mbeya