Ofisi ya Rais-UTUMISHI
08/06/2026
NAIBU KATIBU MKUU UTUMISHI AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUWA MABALOZI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI
Na Antonia Mbwambo-Dodoma
Tarehe 8 Juni, 2026
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kuzingatia maadili ya kazi, kuwa na tabia njema na kuwahudumia wananchi kwa weledi ili kuongeza ufanisi wa huduma za umma utakaochangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Bw. Daudi ametoa rai hiyo wakati akihitimisha mada ya mafunzo kuhusu Usimamizi wa Utendaji Kazi yaliyotolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi hao Juni 8, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.
Bw. Daudi alisema, mafanikio ya Taasisi za Umma hayapimwi tu kwa utekelezaji wa Mipango na Sera, bali pia kwa namna Watumishi wanavyowahudumia Wananchi wanaowategemea katika kupata huduma. Alisisitiza kuwa tabia njema, uadilifu na uwajibikaji ni sifa muhimu zinazopaswa kuonekana kwa kila Mtumishi wa Umma.
“Tunapaswa kutambua kuwa kila Mwananchi anayefika kupata huduma ni mteja muhimu wa Serikali. Jukumu letu ni kuhakikisha anahudumiwa kwa heshima, usikivu na kwa wakati. Hii ndiyo njia bora ya kujenga imani ya Wananchi kwa Taasisi za Umma na kuimarisha utawala bora,” Bw. Daudi alisema.
Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuwa na taifa lenye maendeleo jumuishi, uchumi imara na huduma bora za kijamii, hali ambayo inahitaji Watumishi wa Umma kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kuzingatia maadili na kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Oswin Mkinga, alieleza kuwa usimamizi wa utendaji kazi ni muhimu katika kuboresha matokeo ya Taasisi za Umma kwa kuwa utendaji bora huanza kwa upangaji mzuri wa malengo, ufuatiliaji wa utekelezaji wake na tathmini ya mara kwa mara ili kubaini mafanikio na maeneo yanayohitaji maboresho.
Bw. Mkinga alisisitiza kuwa, usimamizi wa utendaji kazi ni chombo muhimu katika kuimarisha uwajibikaji wa Watumishi na kuongeza thamani ya huduma zinazotolewa kwa Wananchi hivyo, ni lazima kila mtumishi akaelewa mchango wake katika kufanikisha malengo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
02/06/2026
IDHIWANI: SERIKALI YALIPA ZAIDI YA BILIONI 24 MADAI YA WATUMISHI
Aonya Watumishi wanaoghushi barua za uhamisho, Asema 6 mbaroni kesi uhujumu uchumi
Na. Jawadu Kinyobwa
Serikali imeendelea kuboresha ustawi wa watumishi wa umma kwa kulipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya Tsh. Bilipni 24,699,256,645.7 na kulipa watumishi 1,249 waliokoma utumishi yenye thamani ya zaidi ya Tsh. Bilioni 5,548,386,177.90.
Hayo yamebainishwa Juni Mosi, 2026 Mabele Hall jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) katika ufunguzi wa kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara na Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mtaa.
Pamoja na maboresho hayo, Mhe. Ridhiwani amesema wapo baadhi ya waajiri ambao hawatekelezi ipasavyo wajibu wao katika kushughulikia madai ya aina hiyo ambapo hadi kufikia Mei 28,2026 madai ya watumishi 18,021 yenye jumla ya Shilingi 50,917,523,216 hayajawasilishwa Ofisini kwake.
“Baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwasilisha katika Ofisi hii madai yenye kasoro ambazo walipaswa kuzibaini kabla hawajayawasilishwa. Vile vile, yapo madai ya malimbikizo ya mshahara yanayotokana na waajiri kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu na hivyo kuzalisha madeni makubwa kwa Serikali” amesema.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ridhiwani ametoa onyo kali kwa waajiri na viongozi wa taasisi za umma wanaokiuka sheria na taratibu za kiutumishi hususani kwa Waajiri kuchagua aina ya watu wa kufanya nao kazi, kutopokea watumishi wanaohamishiwa kwenye Taasisi zao, Waajiri kujimilikisha Taasisi na kuficha barua zenye maelekezo mahsusi ikiwemo barua za uhamisho.
Sambamba hayo, amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi za Haki Jinai imeanza kuchukua hatua mbalimbali kwa watumishi wanaojihusisha na ukiukwaji wa maadili ikiwemo kughushi barua za Ofisi hiyo ambapo hadi sasa jumla ya watuhumiwa Sita wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya Uhujumu Uchumi na kesi zinaendelea.
Awali akizungumza Katibu Mkuu Ofisi hiyo Juma Mkomi, amesema kikao hicho kimeandaliwa mahsusi kwa lengo la kutathmini nafasi ya wasimamizi wa Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, kubadilishana uzoefu katika kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali hususan katika Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma hasa tunapoelekea kwenye utekelezaji wa Dira Mpya ya Taifa ya 2050.
Pia, Mkomi amesema kikao hicho kitajikita zaidi katika kujadili masuala muhimu ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma, Usimamizi na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA Serikalini, changamoto zilizopo katika utekelezaji wa majukumu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu na namna bora ya kukabiliana nazo.
Kikao kazi hicho kina kauli mbiu isemayo “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Sikivu, Jumuishi, Wenye Matokeo na Uwajibikaji kuelekea Dira 2050”.
28/05/2026
FAIDA ZA KUVAA BEJI KWA WATUMISHI WA UMMA
Click here to claim your Sponsored Listing.
Category
Contact the organization
Telephone
Website
Address
670
Dodoma