The Connect
Hii vita bado mbichi sana.....
11/06/2026
Ilikuwa ni Mei mwaka 2000. Anga la mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, liligubikwa na hofu kubwa. Waasi wa kikundi cha RUF (Revolutionary United Front), walikuwa wameshasonga mbele kwa kasi, wakiteka miji ya kimkakati na sasa walikuwa umbali wa kilomita chache tu nje ya Freetown.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UNAMSIL) vilikuwa vimezidiwa nguvu, na mamia ya walinda amani walikuwa wametekwa nyara na waasi hao. Jiji lilikuwa ukingoni mwa maangamizi makubwa. Kwenye wakati huu wa dharura, nchi ya Uingereza iliamua kuingilia kati. Huu ukawa mwanzo wa Operation Palliser.
Makao makuu ya jeshi la Uingereza, amri ilitolewa: Ondoeni raia wote wa kigeni mara moja. Lengo la kwanza la Operation Palliser halikuwa kupigana vita, bali ilikuwa ni operesheni ya uokoaji (Non-combatant Evacuation Operation).
Kikosi mashuhuri cha makomando wa anga wa Uingereza 1st Battalion, Parachute Regiment (1 PARA) pamoja na meli za kivita k**a HMS Ocean, vilipelekwa kwa kasi ya ajabu hadi Sierra Leone. Ndani ya masaa machache tangu amri hiyo itolewe, helikopta za kijeshi za Uingereza zilianza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Lungi.
Askari wa miamvuli (Paras) walitandaza ulinzi mkali kuzunguka uwanja wa ndege na maeneo ya uokoaji. Raia wa Uingereza, Jumuiya ya Madola, na wageni wengine walioingiwa na hofu walikusanywa na kusafirishwa salama nje ya nchi. Kazi ya kwanza ilikuwa imekamilika kwa mafanikio makubwa.
Baada ya raia wa kigeni kuondolewa salama, Kamanda wa kikosi cha Uingereza, Brigedia David Richards, alikabiliwa na mtihani mzito wa kimkakati. Sheria za operesheni zilimtaka aondoke baada ya uokoaji, lakini alijua fika kuwa akiondoka, Freetown ingeangukia mikononi mwa waasi wa RUF, jambo ambalo lingesababisha mauaji ya kimbari na maangamizi makubwa ya raia wasio na hatia.
Richards alifanya uamuzi wa kijasiri, Kukaa na kuilinda Freetown. Ingawa hawakuwa na mamlaka ya moja kwa moja ya kushambulia kutoka London, Waingereza walibadili mbinu. Walianza kutoa msaada wa kilojistik, kijasusi, na kimkakati kwa jeshi la serikali ya Sierra Leone (SLA) na vikosi vya kikanda. Uwepo wao tu uwanjani uliwarejeshea morali askari wa serikali waliokuwa wamekata tamaa.
Waasi wa RUF, wakiongozwa na mak**anda wao wakatili, waliona uwepo wa Waingereza k**a kikwazo pekee cha wao kutwaa madaraka. Tarehe 17 Mei 2000, kikundi kikubwa cha waasi kilijaribu kushambulia ngome ya Waingereza iliyokuwa Lungi Loi, karibu na uwanja wa ndege.
Huo ulikuwa mtihani wa moto. Waasi walishambulia kwa silaha nzito na RPG. Lakini walikutana na nguvu ya moto kutoka kwa 1 PARA. Ndani ya mapigano hayo mafupi lakini makali, makomando wa Uingereza walizima shambulio hilo kikamilifu, wakawatawanya waasi na kuwathibitishia kuwa Freetown haitachukuliwa kirahisi.
Shambulio hilo lilivunja nguvu na morali ya RUF. Waligundua kuwa hawakuwa wanapigana tena na jeshi lililochoka, bali na moja ya majeshi yenye mafunzo bora zaidi duniani.
Baada ya dhoruba ya kwanza kutulia, Operation Palliser iliongeza kasi. Ndege za kivita za Harrier za Uingereza zilianza kupasua anga la Sierra Leone, zikifanya doria za kuonyesha nguvu (show of force). Milio ya ndege hizi ilitosha kuwatia hofu waasi misituni.
Waingereza walianza pia kutoa mafunzo ya dharura na ya kina kwa jeshi la Sierra Leone (SLA), wakijenga upya mfumo wao wa udhibiti. Hali ilibadilika,jeshi la serikali sasa lilianza kusonga mbele na kuwarudisha nyuma waasi, huku wakisaidiwa na vikosi vya UN vilivyopata nguvu mpya.
Kufikia katikati ya mwezi Juni 2000, hali ya usalama huko Freetown ilikuwa imetengemaa kikamilifu. Hatari ya jiji hilo kutekwa ilikuwa imetoweka, na serikali ilikuwa imerejesha udhibiti wake. Ingawa operesheni rasmi ya Palliser ilihitimishwa tarehe 15 Juni, Uingereza iliacha kikosi cha mafunzo (IMATT) ili kuendelea kuijenga upya Sierra Leone.
Imesimuliwa na
Click here to claim your Sponsored Listing.
Website
Address
Koinange
Nairobi